Familia za waliouawa katika mgodi wa North Mara zinaishitaki LBMA mahakamani kwa kuthibitisha dhahabu inayohusishwa na mauaji yanayodaiwa kutokea
Taarifa ya pamoja kutoka: Action for Southern Africa (ACTSA), CAFOD (Catholic Agency for Overseas Development), Corporate Justice Coalition, Fern, Global Legal Action Network (GLAN), Global Witness, London Mining Network, Mighty Earth, Rights and Accountability in Development (RAID) na Spotlight on Corruption.
Soko la dhahabu la London litakuwa kwenye uchunguzi wa kina kuanzia Oktoba 7 wiki hii katika Mahakama Kuu ya Uingereza, kuhusu uhalali wa madai yake ya upatikanaji wa dhahabu kwa njia zinazozingatia uwajibikaji katika kesi ya kihistoria ya haki za binadamu, dhidi ya LBMA, itakapoanza.
Kesi hii ya kesheria inajaribu kubaini iwapo chombo cha sekta hiyo, ambacho ndiyo kiini cha soko la dhahabu la London lenye thamani ya mabilioni ya dola, kinaweza kuwajibishwa kisheria kwa kuwa na mfumo wa uthibitishaji unaodaiwa kuwa na dosari.
Kesi hiyo imefunguliwa na familia za vijana wawili Watanzania waliofariki katika matukio mawili tofauti ya kupigwa risasi katika mgodi wa dhahabu wa North Mara mwaka 2019. Familia hizo zinasema vijana hao, wote wakiwa na umri wa miaka 23, waliuawa na vikosi vya usalama vilivyokuwa vinalinda mgodi wakati wakitafuta dhahabu. Mwezi Julai, Watanzania wengine 30 walijiunga na mchakato huo wa kisheria, wakidai kuwepo kwa mauaji mengine, kujeruhiwa kwa risasi na kupewa mateso. Madai hayo yamesitishwa kwa muda kusubiri matokeo ya kesi ya mwezi Oktoba.
LBMA inatuhumiwa kuthibitisha kimakosa dhahabu kutoka mgodi wa North Mara nchini Tanzania kuwa ni “safi” na inakidhi viwango vya Responsible Gold Guidance, licha ya kuwepo kwa taarifa za muda mrefu kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaohusishwa na mgodi huo. Mgodi wa North Mara umetajwa kuwa ni miongoni mwa migodi mikubwa inayosababisha vifo vingi zaidi barani Afrika kutokana na vurugu zinazohusiana na masuala ya usalama.
Walalamikaji wanadai kuwa LBMA ina wajibu wa kuwajali watu walioathiriwa na ukiukwaji wa haki za binadamu katika minyororo ya ugavi inayosimamiwa na viwango vyake vya upatikanaji wa bidhaa kwa uwajibikaji, na kwamba LBMA ilishindwa kutekeleza ipasavyo sera zake yenyewe.
“Kesi hii haihusu nani aliyefyatua risasi. Inahusu wajibu wa mfumo wa LBMA wa upatikanaji wa dhahabu kwa uwajibikaji, ambao kwa vitendo uliipa dhahabu ya North Mara hati ya kuwa ‘safi’ licha ya kuwepo kwa mfululizo mrefu wa taarifa zinazodai mauaji, mateso na ukiukwaji mwingine mkubwa. Kesi hii itachunguza iwapo mifumo ya upatikanaji wa bidhaa kwa uwajibikaji ni kinga za kweli au ni ahadi tupu zilizoandikwa kwenye karatasi — na iwapo taasisi za uidhinishaji kama LBMA zinaweza kuwajibishwa pale mifumo wanayoweka majina yao itashindwa.”
– Anneke Van Woudenberg
Kwa zaidi ya muongo mmoja, dhahabu ya North Mara ilisafishwa na MMTC-PAMP nchini India, kampuni ya usafishaji dhahabu iliyoidhinishwa na LBMA chini ya mfumo wa Good Delivery na ambayo ni sehemu ya MKS PAMP Group yenye makao yake Uswisi. Licha ya taarifa za mara kwa mara katika vyombo vya habari na malalamiko kutoka mashirika ya kiraia kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika mgodi huo, LBMA haikusimamisha wala kumuondoa MMTC-PAMP — ingawa wakati huo ilikuwa ikiwataka wasafishaji kusimamisha ununuzi wa dhahabu kutoka kwenye migodi ambayo ilikuwa ikichunguzwa kwa tuhuma za ukiukwaji mkubwa.
Kesi hii inaweka historia mpya kwa kutaka taasisi ya uthibitishaji iwajibishwe kwa madai ya kushindwa katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa kwa uwajibikaji. Madhara na athari zake yanaweza kufika mbali zaidi ya sekta ya dhahabu, na kuibua maswali kuhusu uwajibikaji wa mifumo ya hiari ya uthibitishaji inayotumika katika minyororo ya ugavi duniani.
Mashirika ya kiraia yamekuwa yakitoa tahadhari kwa miaka mingi kuhusu madhaifu kwenye mpango wa LBMA wa upatikanaji wa dhahabu kwa uwajibikaji, yakisema kuwa mpango huo umetumia lebo ya “dhahabu safi” kuficha au kufunika ukiukwaji wa haki, na umeshindwa kuzuia dhahabu inayohusishwa na migogoro, utakatishaji fedha, pamoja na madhara makubwa kwa haki za binadamu na mazingira kuingia katika soko la London.
RAID iliwasilisha malalamiko chini ya ‘Incident Review Process’ ya LBMA mwaka 2020 na 2022, ikirejea matokeo “ya kutia wasiwasi mkubwa” yaliyopatikana katika misheni mbalimbali za utafiti zilizofanyika katika eneo hilo.
LBMA inakanusha dhima. Inasema kuwa haiidhinishi wala kuthibitisha migodi, haina udhibiti juu ya shughuli zinazofanyika North Mara wala juu ya vikosi vya usalama vya Tanzania, na kwamba ilichukua hatua kwa njia inayofaa na yenye mantiki kwa mujibu wa kanuni zake.
Kesi dhidi ya LBMA iliwasilishwa katika Mahakama Kuu ya London mwezi Desemba 2022. Kesi hiyo inaanza katika Mahakama Kuu London tarehe 7 Oktoba 2026 na inatarajiwa kuchukua wiki sita. Walalamikaji wanawakilishwa na Leigh Day, huku Mwanasheria Mkuu wa zamani Dominic Grieve KC akiongoza timu ya mawakili.
Mashirika ya haki za binadamu yatoa kauli
Lucy Brill, Mkuu wa Sera za Sekta Binafsi, CAFOD
“Kwa bahati mbaya, kesi hii si tukio la pekee. Washirika wetu kote duniani mara kwa mara huripoti vitendo vya vurugu na vitisho wanapochukua hatua dhidi ya uchimbaji madini usio na uwajibikaji. Ukiukwaji wa haki za binadamu katika mnyororo wa ugavi si doa linaloweza kung’arishwa na kuondolewa. Viwango dhaifu vya LBMA vinamaanisha kuwa watumiaji na wawekezaji wanaweza kuwa na imani ndogo kwamba dhahabu wanayonunua haijachafuliwa.
“Ikiwa kesi hii itafanikiwa, si tu kwamba wajane wa vijana hawa wawili watapata kiwango fulani cha haki, bali pia itaweka msingi wa kisheria utakaowataka wasimamizi wa mifumo mingine ya uthibitishaji kuchukua majukumu yao kwa uzito. LBMA inahitaji kuweka vikwazo vyenye ufanisi zaidi — ikiwemo kuwaondoa kwenye mfumo — wale wanaokiuka mara kwa mara viwango vya msingi.
“In short, the gold market needs to clean up its act.”
Hannah Mowat, Mshauri wa Masuala ya Misitu na Haki za Binadamu, Fern
“Kwa benki na wafanyabiashara wa vito, LBMA hutoa alama ya ubora inayowahakikishia kwamba dhahabu iliyothibitishwa na taasisi hiyo imepatikana kwa kuzingatia maadili. Bila kujali matokeo ya kesi hii, ukiukwaji mkubwa ambao ni kiini cha kesi hii unaonyesha udhaifu na utupu wa madai kama hayo. Huku mahitaji ya dhahabu yakiongezeka kwa kasi na kuchochea uharibifu wa misitu pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza inapaswa kufuatilia kwa karibu kesi hii. Usimamizi na uangalizi wa kidemokrasia wa kutosha wa sekta hii yenye faida kubwa unahitajika haraka.”
Gearóid Ó Cuinn, Mkurugenzi wa Global Legal Action Network (GLAN)
“Minyororo ya ugavi duniani inategemea mifumo inayotaarifu benki, wawekezaji na wafanyabiashara ni bidhaa zipi wanaweza kuzichukulia kuwa zimepatikana kwa uwajibikaji. Mifumo hiyo haiwezi kuzipa uhalali bidhaa zinazohusishwa na ukiukwaji mkubwa wa haki, halafu ikatae kuwajibika pale uhakikisho huo unapobainika kuwa hauna msingi. Kesi hii inaibua swali pana zaidi: ikiwa taasisi za uthibitishaji zinafanya kazi kama walinzi wa kuingilia masoko ya dunia, ni wajibu gani wa kisheria unaofuata pale walinzi hao wanaposhindwa?”
Diana Salazar, Mratibu wa Amerika Kusini, London Mining Network (LMN)
“LBMA lazima iwajibishwe kwa kutoa muhuri wake wa idhini kwa dhahabu chafu inayohusishwa na ukiukwaji wa haki za binadamu. Tunasimama kwa mshikamano na familia za Watanzania zinazohuzunika kwa kupoteza wapendwa wao na zinazodai haki na uwajibikaji kutoka kwa taasisi inayoongoza katika biashara ya madini ya thamani. Kesi hii inaonyesha umuhimu mkubwa wa kuwa na viwango vikali zaidi ili kukomesha ushiriki wa London katika madhara yanayozikumba jamii zilizoathiriwa na shughuli za uchimbaji madini.”
Sam Mawutor, Mkurugenzi wa Afrika, Mighty Earth
“Viwango vinavyokagua nyaraka kwenye lango la kiwanda cha kusafisha dhahabu lakini havifiki kwenye eneo ambako dhahabu inachimbwa haviwalindi watu walioko kwenye maeneo ya uchimbaji. Kila siku, dhahabu yenye asili ya utata wa kisheria inayotiliwa shaka kutoka Amerika Kusini hadi Afrika huingia katika masoko ya kimataifa, huku nyuma yake ikiacha mito iliyotiwa sumu, misitu iliyoharibiwa, ardhi za kilimo zilizoteketezwa na jamii zilizoharibiwa. Kesi hii inachunguza iwapo mifumo ya ‘upatikanaji wa bidhaa kwa uwajibikaji’ ina maana yoyote, na inaipa LBMA pamoja na taasisi nyingine zinazoweka viwango fursa ya kuziba mianya inayoruhusu dhahabu chafu kuuzwa kama dhahabu safi.”
Helen Taylor, Naibu Mkurugenzi wa Spotlight on Corruption
“Kesi hii inaweka kioo mbele ya minyororo ya ugavi ambayo London imejenga juu yake sifa yake kama kituo kinachoongoza katika biashara ya dhahabu inayowajibika. Huku mahitaji ya dhahabu yakiongezeka kwa kasi, uchunguzi madhubuti na uwajibikaji wa sekta hii yenye nguvu ni muhimu ili kuhakikisha kwamba kutafuta faida hakufanyiki kwa gharama ya watu na mazingira. Kesi hii itapima uaminifu wa viwango vya sekta hiyo, ili kuhakikisha kwamba uthibitishaji wa LBMA hauwezi kutumiwa kama pazia la kuficha rushwa, ukiukwaji wa haki za binadamu au madhara ya kimazingira yanayochafua biashara ya dhahabu duniani.”
Maelezo ya ziada
- Kesi hiyo imepangwa kuendelea kuanzia tarehe 7 Oktoba hadi tarehe 20 Novemba 2026.
- Tazama taarifa zote za LBMA zinazohusiana na kesi hii hapa.
- Mgodi wa North Mara unamilikiwa kwa sehemu kubwa na kampuni ya kimataifa ya Kanada, Barrick Mining Corporation, ambayo ni mojawapo ya kampuni kubwa zaidi za uchimbaji dhahabu duniani. Barrick inakanusha vikali kuwajibika kwa vitendo vya jeshi la polisi.
- Mwezi Julai 2026, serikali ya Uingereza ilitangaza vikwazo vilivyolenga biashara ya dhahabu inayohusishwa na migogoro nchini Sudan.
- Dhahabu inayouzwa kinyume cha sheria itakuwa miongoni mwa mada za kipaumbele katika Mkutano wa Uingereza kuhusu Fedha Haramu, ambao unalenga kukabiliana na mtiririko wa fedha chafu duniani kote na unatarajiwa kufanyika London katika miezi ijayo. Kwa maelezo zaidi, tembelea hapa.

